Jaji wa mahakama kuu ya Milimani Daniel Ogola Ogembo amemhukumu mwanamme wa miaka 36 kifungo cha miaka 40 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Uanasheria.
Hillary Kipkorir Yego alimuua Maxwell Gakure Kariuki tarehe 28 mwezi Juni 2017, kando ya barabara ya Limuru katika Kaunti ya Nairobi.
Wakili wa upande wa mashtaka Mercy Njoroge alifahamisha mahakama kuwa marehemu alikuwa na umri wa miaka 26 wakati wa kifo chake, na alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya uanasheria katika chuo kikuu cha Mount Kenya.
Akitoa hukumu , jaji Ogembo alisema ingawa mshtakiwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa, aliendelea kusisitiza kwamba hakuwa na hatia na hata kutojutia kitendo hicho.
Jaji Ogembo pia aliangazia taarifa ya kabla ya hukumu,iliobainisha kuwa kifo cha Maxwell kiliathiria familia yake.
Aidha jaji aliamua kuwa hukumu hiyo itatekelezwa kuanzia tarehe 24 mwezi juni mwaka 2017,tarehe ambapo mshtakiwa alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mauaji.