Mwanamume anayetuhumiwa kwa kumlaghai mkazi shilingi milioni 3.2 katika sakata ya uuzaji wa ardhi amefikishwa katika mahakama ya Mumias, kaunti ya Kakamega.
Inadaiwa mshukiwa, Benea Bulialia Wangulu, alijisingizia kuwa wakili ili kumlaghai mkazi huyo kwa kusaidiwa na wenzake, akiahidi kuwauzia kipande cha ardhi kilichopo eneo la Panyako Kholera katika eneo bunge la Matungu.
Akifika mbele ya Hakimu Gabriel Otieno, Wangulu alikabiliwa mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulaghai na wizi.
Kulingana na upande wa mashtaka, mtuhumiwa alitekeleza uhalifu huo Novemba 21, 2023 kwa kumshawishi mkazi huyo kulipa kitita kikubwa cha fedha kwa kipande cha ardhi ambacho hakikuwepo.
Ombi la dhamana la mshukiwa kupitia kwa wakili wake Modrix Ondala lilikataliwa na Hakimu aliyeagiza mshukiwa kusalia korokoroni hadi Disemba 31, 2024.
Hatua hiyo inalenga kutoa muda wa kutosha wa kukusanywa kwa ushahidi katika kesi hiyo.
Taarifa ya Carolyn Necheza