Mwanamitandao akamatwa Uganda kwa kumtukana Mfalme Kabaka

Marion Bosire
2 Min Read

Jamaa mmoja maarufu kwenye mtandao wa TikTo raia wa Uganda, ambaye anasemekana kumtukana mfalme Kabaka wa ufalme wa Buganda, Ronald Mutebi na Rais Yoweri Museveni amewekwa rumande katika gereza la Luzira.

Ibrahim Musana maarufu kama Pressure24/7 alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkuu katika barabara ya Buganda kwa madai ya matamshi ya chuki na kusambaza habari za uwongo.

Musana alikana madai yote dhidi yake mbele ya hakimu mkuu Ronald Kayizzi na akawekwa rumande hadiMachi 7, 2024.

Alijikanganya tena kidogo pale alipoomba msamaha na kuahidi kukoma kushambulia viongozi mitandaoni na kufuta video zote za matamshi ya chuki kwenye akaunti yake ya TikTok.

Pressure24/7 alijitetea akisema hakujua kwa kuchapisha video kama hizo atakuwa anavunja sheria na kwamba ana matatizo ya kiakili ikitizamiwa kwamba alilazwa katika hospitali ya walio na matatizo ya kiakili ya Butabika awali.

Alisema pia kwamba anawasiliana na wafalme wa zamani wa ufalme wa Buganda waliofariki ambao kulingana naye wanataka makaburi yao yakarabatiwe ila hana pesa za kufanikisha hilo.

Alikamatwa wikendi iliyopita baada ya uongozi wa ufalme wa Buganda kulalamikia vitendo vyake kulingana na sheria ya matumizi mabaya ya mitandao.

Mahakama ilifahamishwa kwamba kati ya Agosti 2023 na Februari 2024 Musana anayefahamika kama Pressure24/7 kwenye TikTok alichapisha habari za kuchafulia viongozi sifa.

Viongozi hao ni Kabaka Ronald Muwenda Mutebi, Rais Yoweri Kaguta Museveni, Spika wa bunge Annet Anita Among a na waziri wa mawasiliano Joyce Nabbosa Ssebugwawo.

Share This Article