Hali ya huzuni imetanda katika kijiji cha Ogenga kaunti ndogo ya Rachuonyo, kaunti ya Homa Bay baada ya mwanafunzi wa darasa la nane katika shule ya msingi ya Ogenga kujitoa uhai.
Kaimu chifu wa kata ndogo ya Kasewe Dickson Samba, alisema msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 Yvonne Achieng, alijitoa uhai kanisani.
Alisema mwili wa Achieng ulipatikana ukiwa umeningínia katika paa la kanisa siku ya Jumanne huku fulana ikiwa shingoni mwake.
Kulingana na chifu huyo, mwili wa msichana huyo ulipatikana na mamake aliyekuwa akimtafuta baada ya kutoweka nyumbani siku ya Jumatatu.
“Msichana huyo alitoweka nyumbani siku ya Jumatatu. Jamaa yake walianza kumtafuta na kisha kupata mwili wake kanisani,”alisema Samba.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Justus Kucha, alisema wameanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.