Maafisa wa upelelezi huko Isiolo wameimarisha msako kutafuta jamaa aliyekuwa amejihami kwa bunduki na ambaye alimpiga risasi mwakilishi wa wadi ya Burat Nicholas Lorot jana jioni.
Naibu Kamishna wa kaunti ya Isiolo Christopher Siele alithibitisha kisa hicho akielezea kwamba Lorot alikuwa na mwakilishi wa wadi ya Oldonyiro David Lemantile ambaye ni naibu spika wa bunge la kaunti ya Isiolo.
Wawili hao walikuwa katika hoteli ya Northern Galaxy mjini Isiolo wakati Lorot alitoka nje kidogo kupokea simu.
Wakati akiendelea kuzungumza kwa simu ndani ya gari lake, jamaa liyekuwa amevaa helmeti na koti la kung’aa alikuja kwenye dirisha akijaribu kuzungumza naye lakini hakumsikia.
Mwakilishi wadi huyo aliamua kushusha kioo cha mlango wa gari ili wawasiliane lakini jamaa akatoa bastola na kumpiga risasi mbili kabla ya kutoweka.
Risasi hizo zilimpiga kidole na bega lakini hakulegea mara moja aliendesha gari lake hadi kituo cha polisi cha Isiolo akafahamisha maafisa wa polisi kuhusu kisa hicho, kisha wakampeleka katika kaunti jirani ya Meru kwa matibabu.
Siele amefafanua kwamba Lorot hayuko hatarini kwa sasa huku akionya wananchi dhidi ya kukisia kuhusu kisa hicho ili kutoa fursa kwa maafisa wa upelelezi kuchunguza kikamilifu.
Naibu huyo wa kamishna alisema maafisa watakwenda kutafuta video ya kamera za ulinzi kutoka hoteli ya Northern Galaxy wanapojaribu kutambua mshambuliaji.
Ameomba pia walio na taarifa ambazo zinaweza kusaidia kutambua jamaa huyo waziwasilishe kwa maafisa wa upelelezi.