Kamati ya mazungumzo ya maridhiano baina ya serikali na upinzani inatarajiwa kusaini mkataba wa maelewano Jumatano ijayo kabla ya mazungumzo kuanza rasmi.
Haya yameafikiwa leo Ijumaa baada ya mazungumzo kati ya muungano wa Kenya Kwanza na Azimio la Umoja.
Kiongozi wa upinzani kwenye mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka na mwenzake wa serikali Cecily Mbarire ambaye ni gavana wa kaunti ya Embu, wamesema wametoa mwongozo wa mazungumzo hayo.
Mwongozo huo utasainiwa na pande zote Jumatano wiki ijayo kabla ya mazungumzo kungóa nanga rasmi.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo wengi wametilia shaka hatima ya mazungumzo hayo.
Hii ni baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kunukuliwa akisema mazungumzo hayo hayataambulia chochote.
Upande wa upinzani unashinikiza kuzungumziwa kwa masuala yanayofungana na mfumo wa uchaguzi nchini na gharama ya juu ya maisha miongoni mwa masuala mengine.
Hata hivyo, upande wa serikali unashikilia kuwa tayari suala la gharama ya maisha linashughulikiwa na utawala wa sasa na unataja kutolewa kwa mbolea ya bei nafuu inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.