Mvua kubwa ambayo inaendelea kunyesha katika sehemu mbali mbali za nchi, imewasababishia wakazi wengi hasara, baada ya mafuriko kuharibu mali yao.
Mvua hiyo ambayo itaendelea kunyesha wiki hii, imesababisha mito kadhaa kuvunja kingo zake na kuwaacha wakazi wengi bila makao, huku magari mengi yakikumbwa na changamoto za mafuriko barabarani.
Jijini Nairobi, wakazi walitatizika na shughuli za uchukuzi baada ya barabara nyingi kuathiriwa na mafuriko na kusababisha kufungwa kwa barabara hizo.
Shirika la msalaba mwekundu imetuma maafisa wa uokoaji kukadiria hali katika maeneo kadhaa Jijini Nairobi.
“Baadhi ya maeneo yalioathirikana mafuriko Nairobi ni pamoja na Mukuru, Mathare, Huruma, Ruaraka, Baba Dogo, Bosnia, Umoja 3, Choka, Njiru, Ruai, Utawala, Githurai, Kahawa, Eastern Bypass, Kinoo, Kijabe, Limuru, Ruiru, Graceland, Joska, Kaswito, Kicheko, Mangili, Kenyatta Road, Juja, Kitengela, na Magadi” ilisema shirika hilo kupitia mtandao wake wa X.
Katika barabara ya Thika Superhighway, mafuriko yaliyosababishwa na kufurika kwa mto Kamiti, yalikatiza usafiri kati ya chuo kikuu cha Kenyatta na kambi ya jeshi ya Kahawa Garrison.
Hali sawia na hiyo ilishuhudiwa katika maeneo ya Mathare, Ruaka, Kahawa West, Kitengela, Syokimau, Juja, Ruiru, ambapo katika mtaa wa Mathare watu sita wameripotiwa kutoweka.
Mto Athi ambao umevunja kingo zake umesababisha kufungwa kwa barabara muhimu na daraja, na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa, imesema mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa katika sehemu mbali mbali za nchi juma hili.