Mvua kubwa inaendelea kunyesha Uarabuni na kuzua mafuriko yaliyosababisha vifo na kutatiza safari za ndege katika uwanja wa pili wenye shughuli nyingi duniani wa Dubai.
Wasmamizi wa uwanja huo walionya kuwepo kwa matatizo, huku wakiwataka abiria kusubiri kabla ya kufika kwenye uwanja huo, kwani sehemu zake kadhaa zilifurika. Kaskazini mwa uwanja huo mwanamume mmoja alifariki, baada ya gari lake kusombwa na mafuriko.
Huko Oman, waokoaji walipata mwili wa msichana katika sehemu ya Saham, na kufikisha 19 idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko tangu Jumapili.
Hapo jana Jumatano, safari 300 za ndege kutoka na kuingia katika uwanja wa ndege wa Dubai ambao hutumiwa kuunganisha safari nyingi za ndege katika mataifa mengine ulimwenguni, zilifutiliwa mbali kulingana na habari kutoka kwa shirika la safari za ndege la Flight Aware data, huku mamia ya safari zingine zikicheleweshwa.
Aidha wasimamizi wa uwanja huo ambao mwaka jana waliwahudumia abiria milioni 80, ikiwa ni idadi kubwa zaidi baada ya ile iliyohudumiwa na uwanja wa ndege wa Atlanta nchini Marekani, walisema itachukua muda kwa hali ya kawaida kurejelewa.