Mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kipindi cha siku tano zijazo kuanzia siku ya Alhamisi, Machi 19, 2026.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini (KMD), mvua hizo zinatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya milimita 20 hadi Machi 24.
“Ongezeko la mvua hizo linatarajiwa kufikia kilele kati ya Machi 20-23, 2026, kabla ya kupungua Machi 24,” amesema kaimu Mkurugenzi wa KMD kwenye taarifa.
“Ingawa mvua zinatarajiwa kupungua kuelekea kipindi hiki, zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo kadhaa ya nchi.”
Maeneo ambayo hayo ni eneo la Ziwa Victoria, nyanda za juu magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ufa na nyanda za chini mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwemo Nairobi.
KMD inasema mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha zinaibua mashaka katika maeneo kadhaa ya nchi ikiwa ni pamoja na katika kaunti za Turkana, Samburu, Migori, Bungoma, Busia, Kakamega, Vihiga, Pokot Magharibi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia na Nandi.
Kaunti zingine ni Uasin Gishu, Nakuru, Siaya, Kisumu, Homa Bay, Kisii, Kericho, Bomet, Kiambu, Embu, Murang’a, Kirinyaga, Nyandarua, Nyeri, Laikipia, Tharaka Nithi, Meru, Nairobi, Narok, Kajiado, Makueni, Machakos, Taita-Taveta, Kitui, Kwale, Mombasa na Garissa.
Maeneo mengine ya kutilia shaka kutokana na mvua hizo kubwa zinazotarajiwa kunyesha ni sehemu kadhaa za kaunti za Marsabit, Isiolo, Wajir, Mandera na Tana River.
Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inatoa wito kwa wakazi wa maeneo haya kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko yanayoweza kutokea na hali ya kutoweza kuona vizuri.
Watu wanashauriwa pia kutoendesha magari au kutembea kwenye maji yanayosogea au maeneo ya wazi na kutojikinga chini ya miti ili kuepuka kupigwa na radi.
Kadhalika, watu katika maeneo ambayo hukumbwa na maporomoko ya ardhi pia wametakiwa kuchukua tahadhari zaidi hasa katika maeneo ya Mlima Kenya na Aberdares, na maeneo mengine ya vilima.