Muziki wa Gravity Omutujju wapigwa marufuku katika ufalme wa Buganda

Maneno anayotumia kwenye nyimbo zake yametajwa kuwa machafu na yanayokiuka kanuni za kitamaduni za Uganda.

Marion Bosire
2 Min Read
Gravity Omutujju, mwanamuziki wa Uganda

Waziri mkuu wa ufalme wa Buganda Charles Peter Mayiga, ametangaza marufuku ya muziki wa Gravity Omutujju kwenye vyombo vya habari vya ufalme huo ambavyo ni runinga ya BBS na kituo cha redio cha CBS FM.

Kiongozi huyo aliapa kuwajibisha kila mtangazaji binafsi iwapo watakaidi agizo la kutocheza muziki wa Omutujju.

Amri yake ni pigo kwa msanii huyo wa muziki ambaye amekuwa akiangaziwa siku za hivi karibuni kutokana na nyimbo zake zinazosemekana kuwa zenye utata na zinazokiuka maadili.

Mayiga alitangaza uamuzi wake wa kupiga marufuku muziki huo Jumatatu Disemba 9, 2024 baada ya mkutano na mwanamuziki Lord Fred Ssebatta.

Awali, Gravity Omutujjus na Lil Pazo walikuwa wameitwa kwa mkutano na kituo cha kitaifa cha utamaduni cha Uganda kuhusu maudhui yao yenye utata, mkutano ambao ungefanyika katika ukumbi wa kitaifa wa maonyesho.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kuzungumzia nyimbo kama “Okwepicha”, “Enyama”, “Doozi” na “Omunio”, zote za Gravity.

Nyimbo za Lil Pazo zinazozua utata ni “Enkudi” na “Ensujju”.

Kituo cha kitaifa cha utamaduni nchini Uganda kwenye barua iliyotiwa saini na Phina Mugerwa ambaye ni naibu mwenyekiti wa bodi, kilidhihirisha wasiwasi kuhusu maneno ya nyimbo za wasanii hao.

Kulingana na barua hiyo, maneno hayo hayawiani na kanuni za kitamaduni za Uganda na zile za sekta ya ubunifu nchini Uganda.

Athari za nyimbo kama hizo kwa jamii ni jambo la kusikitisha.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *