Aina ya muziki wa Genge ambao asili yake ni Kenya umejumuishwa kwenye tuzo za Grammy. Hii ni baada ya Recording Academy ambayo huandaa tuzo hizo kufanya marekebisho kwenye vitengo vya tuzo hizo na kujumuisha vitengo vitatu vipya. Vitengo hivyo ni “best alternative jazz album”, “best African music performance” na “best pop dance recording” na vitakuwepo kwenye awamu ya 66 ya tuzo hizo itakayoandaliwa mwezi Februari mwaka 2024.
Muziki wa Genge ulianzia katika eneo la California karibu na jiji la Nairobi na umejumuishwa kwenye kitengo cha “best African music performance” pamoja na aina nyingine za muziki kutoka Barani Afrika kama vile Bongo flava kutoka Tanzania, Amapiano kutoka Afrika Kusini, Ndombolo kutoka Congo na nyingine.
Taarifa iliyotolewa jana na usimamizi wa tuzo za Grammy inaashiria kwamba mabadiliko hayo kwenye vitengo vya tuzo yalipigiwa kura na kupitishwa kwenye mkutano wa hivi punde zaidi wa bodi ya wakurugenzi ulioandaliwa mwezi jana.
Afisa mkuu mtendaji wa Recording Academy Harvey Mason jr, alisema kwamba mabadiliko hayo yalichochewa na nia yao ya kuonyesha kujitolea kusikiliza na kushughulikia mahitaji ya wanaohusika kwenye muziki kwa jumla na kujumuisha aina mbali mbali za muziki.