Muungano wa Azimio waunga mkono azma ya Raila kuwania uenyekiti wa AUC

Tom Mathinji
1 Min Read
Kiongozi wa Upinzani Raila odinga.

Muungano wa Azimo la Umoja One Kenya,  umeunga mkono azma ya kinara wake Raila Odinga, kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Africa AUC.

Kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, siku moja baada ya Odinga kutangaza azma ya kuwania wadhifa huo, muungano wa Azimio ulisema utamuunga mkono kikamilifu.

“Muungano wa Azimio unampongeza kinara wake kwa  kuchukua hatua hiyo ya ujasiri ya kuwasilisha jina lake kwa uteuzi wa wadhifa huo muhimu kwa bara la Afrika. Tunaunga mkono hatua aliyochukua,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Muungano huo ulisema kutokana na uongozi wake ulio na maono, utaiwezesha tume ya Umoja wa Afrika kuafikia malengo yake ya bara lenye amani na linalostawi.

Siku ya Alhamisi, Raila alisema yuko tayari kuhudumia bara la Afrika katika wadhifa huo akipewa fursa ya kufanya hivyo.

Akitangaza nia ya kuwania wadhifa huo, Raila alisema amezuru mataifa mengi ya Afrika alipohudumu kama Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu wa AU.

Ikiwa ataidhinishwa na mataifa wanachama 55, Raila atachukuwa wadhifa wa Moussa Faki, na kuelekea Jijini Addis Ababa, Ethiopia, katika makao makuu ya Umoja wa Afrika.

Share This Article