Aliyekuwa Rais wa Malawi Peter Mutharika anatarajiwa kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais nchini nchini humo baada ya kumshinda Rais aliye mamlakani Lazurus Chakwera.
Mutharika aliye na umri wa miaka 85, anaongoza kwa asilimia 57 ya kura zote zilizohesabiwa na tume ya uchaguzi nchini Malawi hadi kufikia Jumanne usiku.
Matokeo hayo yanaashiria kurejea mamlakani kwa Mutharika aliyetimuliwa kwenye wadhifa huo miaka mitano iliyopita baada ya kushindwa na Chakwera kwenye uchaguzi mkuu.
Kulingana na tume ya uchaguzi, mshindi wa kinyang’anyiro hicho ni sharti apate asilimia 50 na kura moja kati ya kura zote zilizopigwa.
Inaaminika Chakwera amepoteza umaarufu kutokana na kutotimiza ahadi zake za kabla ya uchaguzi, ikiwemo kufufua uchumi wa nchi hiyo.