Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametoa onyo kali kwa wale ambao wanajiandaa kwa maandamano kesho Jumanne, Julai 23, 2024.
Museveni ameonya kwamba waandamanaji hao “wanacheza na moto” iwapo wataendeleza mipango yao ya kuandamana kulalamikia kile walichokitaja kuwa ufisadi.
Katika mitandao ya kijamii, vijana nchini humo wamekuwa wakiandaa maandamano wakisema kilichowachochea ni ufisadi uliokithiri serikalini.
Inaaminika vijana hao wametiwa motisha na maandamano ambayo yamekuwa yakitekelezwa nchini Kenya na vijana wenzao wa Gen Z ambao pia wanashinikiza utawala bora.
Katika taarifa iliyopeperushwa kwenye runinga nchini Uganda, Rais Museveni aliwaonya waandalizi wa maandamano kwamba mpango wao hautakubalika wala kustahimiliwa.
“Tunajitahidi kuongeza uzalishaji wa mali nchini, nanyi mnataka kutusumbua. Mnacheza na moto kwa sababu hatutakubali mtusumbue,” alifoka Museveni kwenye hotuba yake.
Alilaumu waandalizi wa maandamano hayo kwa kile alichokitaja kuwa ushirikiano na mashirika na watu kutoka mataifa ya kigeni kusababisha vurugu nchini Uganda.
Nchini Kenya vile vile, mashirika ya nchi za nje yamekuwa yakilaumiwa kwa kufadhili maandamano ya Gen Z hasa Wakfu wa Ford ambao serikali ya Kenya iliuandikia waraka kutaka kujua jinsi fedha ambazo wakfu huo ulitoa kwa mashirika ya humu nchini zilitumika.