Museveni asema bado anazingatia kanuni za Covid-19

Marion Bosire
2 Min Read
Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefichua kwamba bado anafuata taratibu za kudhibiti maambukizi ya virusi vya korona, Covid-19, takriban miaka minne tangu masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo yaondolewe nchini humo.

Rais huyo alielezea kwamba bado anaendelea kufanya sehemu kubwa ya kazi zake za kila siku akiwa nje kwa kuzingatia kanuni za kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Jana Jumapili asubuhi, kiongozi huyo alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuadhimisha miaka 100 ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Rubaga.

Alifika kwa wakati, akilakiwa na viongozi wa kanisa wakiwemo Askofu Mkuu wa Kampala, Paul Ssemogerere.

Hata hivyo, Museveni hakukaa ndani ya jengo kuu pamoja na waumini wengi. Badala yake, alikaa nje wakati wa ibada, akiwahutubia wageni waliokusanyika kutoka kwenye hema lililowekwa uwanjani.

Katika hotuba yake, Rais huyo alisema, “Ninamshukuru Askofu Mkuu kwa kuniruhusu niwahutubie nikiwa hapa nje,” alisema Museveni.

“Tangu kipindi cha Korona, utaratibu wetu wa kawaida ni kwamba siingii ndani ya maeneo yaliyofungwa na kukaa humo. Naingia na kutoka, kama vile katika mbinu zetu za kivita za msituni.”

Kando na kutokaa katika maeneo yaliyofungwa ya watu wengi, Museveni na mkewe Janet mara nyingi huvaa barakoa wanapokwenda katika maeneo ya umma.

Rais Museveni anaendeleza kampeni anapowania muhula wa saba afisini kama kiongozi wa taifa hilo, akiahidi kwamba utakuwa wake wa mwisho.

Website |  + posts
Share This Article