Kamati ya Kiufundi yenye Wanachama kutoka Sekta Mbalimbali imemkabidhi Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen ripoti yake yenye mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuboresha utendakazi wa viwanja vya ndege nchini.
Murkomen aliiteua kamati hiyo kuchunguza hali ya viwanja vya ndege nchini kufuatia kuchipuka kwa habari za kuvuja kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.
Kamati hiyo iliongozwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini, KAA Mhandisi Walter Ogolla na ilikuwa na siku 35 kutayarisha ripoti yake.
Kamati hiyo ilichunguza hali ya viwanja vya ndege vya JKIA, Moi na Wilson.
“Timu hiyo ilifanya kazi maridhawa na kutoa mapendekezo muhimu ambayo yataongoza utekelezaji marekebisho katika viwanja vyetu vya ndege siku zijazo,” alisema Murkomen baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo.
“Ripoti hiyo unganishi inaangazia masuala yote kwa kina.”
Mojawapo ya mapendekezo makuu ya ripoti hiyo ni kwamba KAA inapaswa kuajiri maafisa zaidi kupunguza pengo la rasilimali watu ambalo limekuwa changamoto ya muda mrefu.
Mamlaka hiyo imekuwa ikikabiliwa na watu mgumu kutokana na wafanyakazi wasiokuwa na mpangilio na motisha ya kuchapa kazi. Pendekezo la kamati hiyo kuwa mikataba iliyopo sasa ipitiwe upya limetajwa kuwa muhimu na linatazaliwa kubadili hali hiyo.
Kwa upande mwingine, pendekezo la kamati hiyo kwamba mikataba itolewa kulingana na kiwango cha utendakazi linatarajiwa kuboresha mno utoaji huduma na kuhakikisha uwajibikaji, viwango vya juu vya utendakazi na thamani ya fedha zinazolipwa na walipaji kodi.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuwepo haja ya kuboresha barabara katika viwanja vya ndege, maegesho ya magari, kukarabati paa zinazovuja na uboreshaji wa vituo vinavyotumiwa na wasafiri.
Kamati hiyo pia imependekeza kukarabatiwa kwa barabara za ndege ambazo zimechakaa.