Aliyekuwa Gavana wa Meru Peter Munya amesema Mswada wa Fedha wa mwaka 2024, utawaongezea Wakenya mzigo ambao kwa sasa wanakumbwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Akizungumza katika kaunti ya Meru, Munya alidokeza kuwa mapendekezo mengi katika mswada huo hayalengi kuimarisha uchumi wa taifa hili, lakini yatasambaratisha biashara na kuzidisha mzigo kwa wananchi.
Kulingana na Waziri huyo wa zamani wa kilimo, serikali ya Kenya Kwanza imeenda kinyume cha ahadi zake ilizotoa za kuimarisha uchumi, kwa kubuni sera ambazo zinawaumiza wananchi wa kawaida.
Alitoa wito kwa serikali kushughulikia maswala yanayowaathiri Wakenya, na kutilia maanani maoni ya Wakenya kabla ya kuchukua hatua zozote.
Matamshi ya Munya yanajiri huku kamati ya bunge kuhusu bajeti ikikamilisha vikao vya kupokea maoni ya umma kuhusu Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.
Mswada huo umeibua hisia mbalimbali kutoka kwa Wakenya, wengi wao wakisema utasababisha hali ngumu ya kiuchumi hapa nchini.