Munya aunga mkono kubanduliwa afisini kwa Gavana Mwangaza

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa zamani wa kilimo na mmoja wa viongozi katika muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya Peter Munya ameunga mkono kubanduliwa afisini kwa Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza.

Kulingana naye, hatua iliyochukuliwa na wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Meru ni sahihi na inafaa iwapo kiongozi hawajibiki.

Anasema ni vyema kiongozi kama huyo aondoke afisini kutoa fursa kwa viongozi watenda kazi huku akitangaza azma ya kuwania ugavana katika kaunti ya Meru kwenye uchaguzi wa mwaka 2027.

Wakati wa uzinduzi wa usajili wa wanachama wapya wa chama cha PNU na ufunguzi wa afisi za chama katika sehemu mbali mbali nchini, viongozi wa chama hicho waliunga mkono azma yake ya kuwa Gavana wa Meru mwaka 2032.

Wakati huo huo, Munya amekashifu uhitimu wa kimasomo wa waziri wa madini na uchumi wa majini Ali Hassan Joho akisema serikali inadhoofisha mfumo wa elimu nchini.

Aliongeza kusema kwamba alama ya D- katika mtihani wa kidato cha nne KCSE kamwe haiwezi kubadilishwa na kuwa shahada.

Hata hivyo mtaalamu wa elimu ambaye pia ni mwalimu mkuu wa taasisi ya kitaifa ya mafunzo ya kiufundi ya Meru Anderson Mutembe Kirige, amepinga maoni ya Munya.

Kulingana na Kirige, mfumo wa elimu wa sasa nchini unatoa fursa kwa mtu kuendeleza masomo kuanzia kwa kozi za kiufundi, sta shahada na hata kiwango cha shahada ya uzamili.

Share This Article