Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro leo Ijumaa, amepiga marufuku usafirishaji, usambazaji, uuzaji na utumizi wa Muguka katika kaunti hiyo.
Gavana huyo ameagiza idara za utekelezaji sheria za kaunti hiyo, kuhakikisha marufuku hayo yanatekelezwa kikamilifu.
Aidha Mung’aro alitoa onyo kwa afisa yeyote atakayepatikana akishirikiana na watakaokiuka marufuku hayo, kwamba atachukuliwa hatua za kisheria na zile za kinidhamu.
Hatua hiyo ilitarajiwa, baada ya Gavana huyo mnamo mwezi Machi mwaka huu, kuapa kupiga marufuku utumizi wa Muguka katika eneo hilo, akitaja madhara yake hatari.
Alisikitika kuwa utumizi wa bidhaa hiyo, umewaadhiri vibaya vijana wa eneo hilo.
“Hatuna tatizo kama kaunti wakati watu wanaleta na kuuza Miraa, lakini katika kaunti ya Kilifi nitapiga marufuku Muguka na liwe liwalo,” alisema Gavana Mungaro.
Kufuatia agizo hilo, maeneo yote ya kuuza Muguka katika kaunti hiyo yatafungwa mara moja.
Wakati huo huo, magari ya kusafirisha Muguka, hayataruhusiwa kuingia katika kaunti hiyo.
“Idara zote za kaunti zimeagizwa kuhakikisha marufuku hayo yanatekelezwa bila ubaguzi,” aliagiza Gavana huyo.
Munga’ro anafuata nyayo za mwenzake wa Mombasa Abdulswammad Nassir, ambaye alipiga marufuku bidhaa hiyo siku ya Alhamisi.
Akitoa marufuku hayo, katika hospitali ya Port Reitz, Gavana Nassir alisema Muguka inaongoza katika kuzidisha uraibu katika eneo hilo.
Aidha, Gavana huyo alisema serikali ya kaunti yake itatoa huduma za urekebishaji tabia na matibabu kwa waraibu wa bidhaa hiyo bila malipo katika taasisi za afya za kaunti hiyo.