Mudavadi: Wanawake 100 waliuawa Agosti-Novemba, 2024

Martin Mwanje
1 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri

Jumla ya wanawake 100 waliuawa kati ya mwezi Agosti hadi Novemba mwaka huu. 

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi anasema kutokana na hali hiyo, Inspekta Mkuu wa Polisi amebuni Kitengo cha Watu Wasiojulikana Waliko ili kusaidia kukabiliana na  mauaji ya wanawake nchini.

Mudavadi ambaye pia ni kaimu Waziri wa Usalama wa Taifa anasema kufikia sasa, Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imehitimisha uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo na kesi kuwasilishwa mahakamani.

Akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi wakati akiitarifu nchi juu ya mipango ya usalama wakati wa msimu huu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, Mudavadi ameongeza kuwa jopokazi maalum la rais la kutafuta mbinu bora za kukabiliana na mauaji ya wanawake nchini litachapishwa hivi karibuni katika gazeti rasmi la serikali.

Jopokazi hilo litatakiwa kuwasilisha mapendekezo yake ndani ya siku 90 punde baada ya kuanza kuhudumu..

Amedokeza kuwa visa 7,107 vya kingono na dhuluma za kijinsia vimeripotiwa nchini tangu mwaka wa 2023.

Amelalamikia idadi hiyo anayosema ni ukiukaji wa haki za hasa wanawake nchini.

Kaunti ya Nairobi ndio inayoongoza katika visa hivyo huku idadi ndogo ya visa ikiripotiwa katika kaunti za Samburu na Mandera.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *