Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amepongeza ushirikiano kati ya Kenya na Shirika la kimataifa la Hazina ya Ustawi wa Kilimo (IFAD), akisema utasaidia kuimarisha kilimo kinachohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kulingana na Mudavadi, ushirikiano huo utaongeza uzalishaji wa kilimo na kuboresha maisha ya wakulima wa mashamba madogo madogo pamoja na jamii zilizo vijijini.
“Wakati wanakulima wananawiri, Kenya inastawi, utoshelevu wa chakula unashuhudiwa na kuwafaidi wanaolisha taifa hili,’ alisema Mudavadi.
Akizungumza alipompokea Mkurugenzi Mpya wa IFAD hapa nchini Kenya Matteo Marchisio, Mudavadi aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje, alisema ushirikiano huo utawawezesha wakulima kupata mavuno yaliyoimarika, mapato ya juu na fursa zaidi kwa vijana katika kilimo biashara.
Kwa upande wake, Marchisio alisema IFAD itaendelea kushirikiana na serikali ya Kenya pamoja na wadau wengine kuimarisha maisha ya jamii mashinani na kupanua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.
“IFAD imejitolea kupiga jeki utoshelevu wa chakula na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Marchisio.