Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliye pia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amesema shilingi bilioni 607 zitatumwa hapa nchini kutoka ughaibuni mwaka huu.
Mudavadi alisema kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 50 kutoka kile kilichotumwa nchini mwaka 2022, huku pia kukiwa na zaidi ya mikataba 30 ya biashara na uwekezaji itakayotiwa saini.
Kulingana na Mudavadi, mikataba hiyo itajumuisha ile ya kuwaajiri wakenya katika nchi mbalimbali.
Akizungumza afisini mwake katika makao makuu ya shirika la reli jijini Nairobi, Mudavadi alisema kuwa jumbe 24 za biashara na uwekezaji zimetekelezwa, kama sehemu ya jumbe zilizoshirikishwa za biashara na uwekezaji humu nchini na nje ya nchi.
Alisema kuwa Kenya imekamilisha mashauriano na kutia saini mkataba wa kuwaajiri wakenya na ujerumani, na kwamba kwa sasa mashauriano yanaendelea kuhusu mkataba wa kuwaajiri wakenya na nchi za Qatar, Saudi Arabia, Canada na Austria.