Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ameelezea kufurahishwa kwake na hatua ya Rais William Ruto kuongeza wigo wa majukumu yake.
Katika mabadiliko ya kwanza ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Ruto jana Jumatano, Mudavadi sasa atasimamia Ofisi ya Waziri mwenye Mamlaka Makuu na Wizara ya Mambo ya Nje.
“Nahongera zaidi na kunyenyekea kutokana na hatua ya Rais William Ruto kupanua majukumu yangu kwa kuniongezea jukumu lingine muhimu la Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema Mudavadi katika taarifa leo Alhamisi.
“Ninafahamu umuhimu wa majukumu hayo mawili, na ninayakumbatia kwa hisia ya kujituma. Naahidi kuendelea kuwahudumia Wakenya na nchi yetu kwa kujitolea vilivyo, na kwa uadilifu na uangalifu. Nitatetea na kulinda maslahi ya Wakenya ndani na nje ya nchi. PAMOJA TUDUMISHE HADHI YA KENYA NDANI NA NJE YA MIPAKA YETU,” aliongeza Mudavadi.
Katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri, Dkt. Alfred Mutua alihamishwa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na sasa atahudumu kama Waziri wa Utalii na Wanyama Pori, wadhifa ambao awali ulishikiliwa na Peninah Malonza.
Malonza sasa ametwikwa jukumu la kuongoza Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda ambayo awali ilishikiliwa na Rebeccah Miano.
Miano sasa anarithi wadhifa ulioshikiliwa na Moses Kuria wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda na pia amemshukuru Rais Ruto kwa kumtwika wadhifa huo mpya.
“Asante Rais William Ruto kwa uaminifu na fursa hiyo ya thamani. Ni kwa taadhima na unyenyekevu ambapo nachukua wadhifa wangu mpya katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda. Nimejitolea kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kama ilivyoelezwa katika Ajenda ya Maendeleo ya Kiuchumi kutokea Chini hadi Juu na kuleta maendeleo kwa watu wa Kenya,” alisema Miano wakati akizungumzia uteuezi wake mpya.
Kuria ambaye amekuwa akishtumiwa mara kwa mara kutokana na semi zake tatanishi sasa amehamishiwa Wizara ya Utumishi wa Umma, Utendakazi na Usimamizi wa Utoaji Huduma, wizara ambayo awali ilishikiliwa na Aisha Jumwa ingawa imefanyiwa mabadiliko kidogo.
Jumwa sasa atahudumu kama Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi, hii ikiwa ni wizara mpya.
Waziri wa Maji Alice Wahome ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akilumbana na Katibu katika wizara hiyo pia amehamishwa katika mabadiliko hayo.
Wahome sasa ameteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji akibadilishana himaya na Zacharia Njeru ambaye ameteuliwa kumrithi katika Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyiziaji Maji Mashamba.