Mudavadi: Maeneo maalum ya kiuchumi yatabuni nafasi za ajira

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi azuru eneo maalum la kiuchumi la Tatu City.

Maeneo maalum ya kiuchumi ni muhimu sana katika kutimiza malengo ya serikali ya Kenya kwanza ya kubuni nafasi za ajira, kuwawezesha vijana na maendeleo ya taifa, amesema waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Mudavadi alisema serikali imejitolea kubuni mazingira bora yanayovutia uwekezaji na kubuni nafasi za ajira miongoni mwa vijana.

Akizungumza leo Jumamosi alipozuru eneo la kiuchumi la Tatu City, Mudavadi alisema miradi kama vile Tatu City ni muhimu katika kupiga jeki maendeleo ya taifa.

“Tatu City ni mfano bora wa miradi ambayo inakusudiwa kutekelezwa kote nchini. Mradi huu ni kuhusu kubuni nafasi, kuwawezesha vijana na kujenga mustakaba wa taiofa hili utakaowafurahisha wote,” alisema Mudavadi.

Katika ziara hiyo, Mudavadi aliangazia sana umuhimu wa kubuni fursa kwa vijana wa hapa nchini kupitia eneo hilo maalum la kiuchumi la Tatu City.

Mudavadi alishauriana na usimamizi wa Tatu City ukiongozwa na Stephen Jennings, kuhusu jinsi mradi huo unabadilisha uchumi wa taifa hili.

“Hapa kuna fursa tele ambazo ni nguzo kuu kuwawezesha vijana wetu ambao ni uti wa mgongo wa mustakabal wa taifa hili,” alidokeza waziri huyo wa mambo ya nje.

Share This Article