Mudavadi kumwakilisha Rais Ruto Zimbabwe

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi anaondoka nchini leo kuelekea jijini Harare nchini Zimbabwe ambako anakwenda kumwakilisha Rais William Ruto kwa sherehe ya kumwapisha Rais Emerson Mnangagwa Jumatatu Septemba 4, 2023.

Taarifa kutoka kwa afisi ya waziri huyo inaelezea kwamba ziara yake nchini humo ni ya siku mbili huku ikitaja uhusiano mwema ulioko kati ya nchi hizi mbili na kwamba Kenya inampongeza Mnangagwa kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

Taarifa ya Mudavadi imesheheni ujumbe wa Rais Ruto wa pongezi kwa Mnangagwa ambao ni, “Kwa niaba ya serikali na watu wa Kenya, Rais William Ruto anapongeza Rais mteule Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

Rais anapongeza watu wa taifa la Zimbabwe kwa kutekeleza uchaguzi kwa njia ya amani na kwamba Kenya inajitolea kuendelea kudumisha uhusiano mwema na serikali na watu wa Zimbabwe.”

Taarifa hiyo imetiwa saini na msimamizi wa mawasiliano katika afisi ya waziri aliye na mamlaka makuu Salim Swaleh.

Mnangagwa alishinda kwa asilimia 52.6 ya kura zilizopigwa majibu ambayo yanapingwa na upande wa upinzani nchini humo.

Kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo, mpinzani wa Mnangagwa, Nelson Chamisa, alipata asilimia 44 ya kura zilizopigwa.

Mnangagwa wa umri wa miaka 80 aliingia kwenye uongozi wa nchi hiyo wakati Robert Mugabe, alibanduliwa kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Chama chake cha ZANU-PF kimeongoza nchi hiyo kwa miaka 43 sasa.

Share This Article