Mudavadi kumwakilisha Rais Ruto Denmark

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje anatarajiwa nchini Denmark leo kwa mkutano wa viongozi wa ngazi za juu kuhusu ushirikiano kati ya Denmark na Afrika.

Mudavadi anamwakilisha Rais William Ruto kwenye mkutano huo wa kujadili masuala muhimu ya uhusiano wa Denmark na Afrika. Ataandamana na balozi wa Kenya nchini Denmark Angeline Musili na wajumbe wengine.

Mkutano huo unalenga kushughulikia sera mpya ya Denmark inayozingatia nguzo tatu za biashara na uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi, na amani na usalama.

Kulingana na Musili, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wadau 200 wa ngazi za juu kutoka bara la Afrika.

Awali, Mudavadi alishauriana na balozi wa Denmark nchini Kenya Stephan Schønemann afisini kwake kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo muhimu.

Mudavadi na Schønemann walijadili uimarishaji wa biashara, uwekezaji na uhusiano wa kitamaduni kati ya nchi hizo mbili.

Mudavadi anaamini kwamba kuimarisha uhusiano na Denmark ni muhimu kwa maendeleo ya Kenya na ufanisi wake kiuchumi.

Share This Article