Waziri mwenye mamlaka makuu, aliye pia waziri wa mashauri ya kigeni Musalia Mudavadi ataondoka nchini juma hili kuelekea mjini Beijing nchini China.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China Wang Wenbin, alithibitisha siku ya Jumanne kuwa Mudavadi atafanya ziara rasmi nchini humo kuanzia tarehe 24 hadi 26 mwezi huu wa Januari.
Ziara hiyo inajiri baada ya mwaliko wa kamati kuu ya chama cha kikoministi, kinachotawala nchini China, na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Wang Yi.
Ziara hiyo ya Mudavadi inajiri miezi michache baada ya Rais William Ruto, kuongoza ujumbe wa Kenya kuzuru China, ambapo maafikiano kadhaa katika nyanja mbali mbali yalitiwa saini.
Mataifa haya mawili chini ya uongozi wa Rais William Ruto na Rais Xi Jinping, yamejitolea kuimarisha uhusiano baina yao.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa China Wang Yi alizuru humu nchini mwaka jana ambapo alikariri kwamba China itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Kenya.