Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, amesema kwamba Kenya itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi nyingine katika azima ya kuafikia amani ulimwenguni.
Mudavadi aliyasema hayo alipohutubu kwenye kongamano la usalama la Munich jijini Nairobi ambalo lililoongozwa na Balozi Christoph Heusgen.
Kongamano hilo liliwaleta pamoja viongozi wa nchi za Afrika na washirika kutoka ughaibuni kujadili njia za kubuni ushirikiano katika amani kwa nia ya kushughulikia changamoto za kisasa za usalama.
Mudavadi alisema hatua ya Kenya imechochewa na ongezeko la vitisho vya usalama na changamoto ambazo hubadilika kila siku kwa kiwango cha kutisha.
“Kufikia hapa, ipo haja kwa nchi zote kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa njia ya ukweli na uwazi.”