Kenya inatarajiwa kuwa mwenyeji wa afisi tatu mpya za Umoja wa Mataifa kufikia mwishoni mwa mwaka ujao, huku Nairobi ikitarajiwa kuwa kitovu cha shughuli za Umoja wa Mataifa (UN).
Baadhi ya afisi zinazotarajiwa kufunguliwa hapa nchini, ni pamoja na afisi ya Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (UNICEF), ile ya Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu (UNPF), na ile ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake (UN Women).
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi wakati wa mkutano wa mashauriano afisini mwake, alisema kutokana na Kenya kuwa katika eneo mwafaka kufanikisha uchukuzi na mipango ya kifedha, kunatoa fursa nzuri kupiga jeki majukumu muhimu ya diplomasia na maswala muhimu ya kikanda na dunia ya UN.
“Tunashirikiana kwa karibu, na Kenya itazamia uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kuifanya Nairobi kuwa kitovu muhimu cha shughuli za UN hapa nchini, kanda na duniani kwa jumla,” alisema Mudavadi.
Tayari Umoja wa Mataifa una afisi mbili hapa nchini, ikiwemo ile ya Mazingira UNEP,na ile kuhusu makazi UN-HABITAT, zote zikiwa Jijini Nairobi.
Mudavadi aliyasema hayo Jumatano, alipokutana na Rais wa kikao cha 79 cha Baraza la Umoja wa Mataifa Philemon Yang, aliyemtembelea afisini mwake.
Kwa upande wake Yang aliishukuru serikali ya Kenya kwa kuikaribisha UN Jijini Nairobi.
“Naishukuru serikali ya Kenya kwa kuipokea Umoja wa Mataifa Jijini Nairobi,” alisema Yang.
Mkutano huo uliwaleta pamoja washirika muhimu kutoka afisi za Umoja wa Mataifa Jijini Nairobi, wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa afisi za UN Nairobi.