Kenya imekanusha madai kwamba ilihusika katika kubuniwa kwa serikali sambamba nchini Sudan.
Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliyepia waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, alibainisha kuwa mkataba uliotiwa saini katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa KICC na kundi la Sudan Rapid Support Forces (RSF), hauhusiani kamwe na kubuniwa kwa serikali sambamba nchini Sudan.
“Kuhusiana na Sudan, nafafanua kwamba hakuna serikali sambamba iliyobuniwa nchini Kenya. Msimamo wetu unasalia kuwa dhabiti, tunaunga mkono amani na udhabiti nchini Sudan,” alisema Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo Jumanne, wakati wa mkutano na mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa Jijini Nairobi, ambapo alidokeza kuwa Kenya imejitolea kuhakikisha usalama na amani, ushirikiano kote duniani na utangamano wa kikanda zinakuwa nguzo za ustawi.
Mudavadi alithibitisha historia ya Kenya kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika michakato ya amani Barani Afrika, huku akitoa mfano wa jukumu muhimu lililotekelezwa na Kenya katika mataifa ya Angola, Sudan Kusini na Somalia.
Waziri huyo alithibitisha kujitolea kwa Kenya kuunga mkono shughuli za kibinadamu nchini Sudan, licha ya hatua ya hivi majuzi ya Sudan kusitisha uagizaji wa bidhaa kutoka Kenya, ikiwa ni pamoja na chai.