Mudavadi azuru Wizara ya Usalama wa Kitaifa, ataarifiwa hali ya usalama nchini

Martin Mwanje
1 Min Read
Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje leo Jumanne ametembelea Wizara ya Usalama wa Kitaifa na kupewa taarifa juu ya hali ya usalama ilivyo kwa sasa kote nchini.
Mudavadi ameteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu kama kaimu Waziri wa Usalama wa Kitaifa kufuatia kuteuliwa na kuapishwa kwa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
Prof. Kindiki amehudumu kama Waziri wa Usalama wa Kitaifa tangu kubuniwa kwa serikali ya Kenya Kwanza.
Wakati wa mkutano na Katibu Dkt. Raymond Omollo, Mudavadi pia alijuzwa mipango inayotekelezwa na wizara hiyo kote nchini.
Waaidha wawili hao walizungumzia wajibu muhimu unaotekelezwa na wizara hiyo katika utekelezaji wa mipango na miradi ya serikali ambayo ina manufaa makubwa kwa taifa.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Mudavadi kutembelea wizara hiyo tangu kuteuliwa kwake kuwa kaimu Waziri wa Usalama wa Kitaifa.
Share This Article