Mudavadi awasili Uganda kwa kongamano la kahawa

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi amewasili jijini Kampala nchini Uganda kwa awamu ya pili ya kongamano la viongozi wa nchi za Afrika, G25 kuhusu kahawa.

Kongamano hilo linaandaliwa na serikali ya Uganda kupitia kwa wizara yake ya Kilimo, mifugo na uvuvi kwa ushirikiano na shirika la kahawa la Afrika – IACO, kati ya Agosti 7 na 10, 2023 katika hoteli ya Speke huko Munyonyo jijini Kampala nchini Uganda.

Mabadiliko katika sekta ya kahawa kupitia kuongeza thamani yataangaziwa kwenye kongamano hilo ili kusuluhisha changamoto zilizopo katika sekta hiyo na kustawisha uzalishaji, utafiti, uafikiaji wa masoko na matumizi ya kahawa katika bara hili.

Awamu ya kwanza ya kongamano la kahawa la G25 iliandaliwa Nairobi, Kenya Mei, 2023, ambapo viongozi wa nchi 25 zinazozalisha kahawa walijitolea kupanga makubaliano ya kuorodhesha kahawa kama mojawapo ya bidhaa muhimu za kilimo katika umoja wa Afrika kulingana na ajenda ya Afrika ya mwaka 2063.

Sekta ndogo ya Kahawa nchini Kenya ni nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa ambapo inachangia asilimia 0.28% ya pato jumla kulingana na utafiti wa kiuchumi wa mwaka 2021.

Zao hilo ni chanzo cha ajira, linahimiza uwepo wa chakula nyakati zote na huchangia kwa kipato cha wakenya wengi. Kahawa ina manufaa kwa wakenya wapatao milioni 5.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *