Kenya imedhibitisha kujitolea kwake kuunga mkono kuanzishwa kwa utaratibu wa utoaji fidia kwa waathiriwa wa dhulma za jadi za utawala wa kikoloni, katika juhudi za kuafikia Muungano wa Afrika.
Waziri mwenye mamlaka Makuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi, alitoa wito kwa mataifa ya bara la Afrika kuweka misingi ya kisheria na kimaadili ya ulipaji fidia akisema bara hili linapaswa kumakinika na mbinu tofauti za utoaji haki ya kulipa fidia kwa waathiriwa.
Mudavadi alitoa wito wa umoja miongoni mwa waafrika hasa katika mataifa ya ugaibuni, kupitia mpango wa pamoja wa utoaji haki ya fidia.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa Afrika kuhusu utoaji fidia jijini Accra Ghana, aliko mwakilisha rais William Ruto.
Mkutano huo unaohudhuriwa na marais na viongozi wa serikali wa bara Afrika unalenga kutoa nafasi ya kuagaziwa kwa maafikio ya mataifa ya bara Afrika kwa pamoja kukabiliana na mathara ya dhulma za kikoloni na ubaguzi wa rangi, dhamira kuu ikiwa ni kuregesha hadhi ya bara Afrika na kuunda mustakabali wa kiafrika.
Mudavadi aliongeza kuwa Kenya kwa upande wake inaunga mkono kuundwa kwa kamati ya afrika ya wataalam kuhusu ulipaji fidia katika juhudi za kustawisha mfumo wa pamoja wa utoaji fidia.
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, alifungua rasmi mkutano huo.