Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesisitiza umuhimu wa kandarasi za utendakazi akisema kandarasi hizo huelezea malengo ya kimkakati ya serikali na ni kipimo cha malengo yanayopaswa kufikiwa katika ngazi mbalimbali za utumishi wa umma.
Amesema kandarasi za utendakazi zinalenga kuimarisha usalama wa umma wakati zikiboresha utoaji huduma kwa raia.
“Kupitia kandarasi hizi, tunasisitiza dhamira yetu ya kukuza malengo ya maendeleo ya Kenya na kuboresha maisha chini ya Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA), kuhakikisha kuafikiwa kwa matokeo yanayowiana na vipaumbele vyetu vya taifa, kuhakikisha ubora, uwazi na matokeo yanayoweza yakadhihirika katika utumishi wa umma,” alisema Mudavadi.
Aliongeza kuwa zoezi hilo la kila mwaka ni msingi wa uwajibikaji na linatoa mpangokazi wa kufuatilia hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya serikali na utekelezaji wa sera.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje aliyasema hayo leo Jumatatu asubuhi alipoongoza zoezi la utiaji saini wa kandarasi za mwaka 2024-2025 akiwa pamoja na Katibu wa Idara Masuala ya Mambo ya Nje Roseline Njogu katika Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri katika Makao Makuu ya Railways jijini Nairobi.