Mudavadi ashutumu maandamano ya sabasaba

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi ameshtumu maandamano ya Saba Saba yaliyoitishwa na upinzani.

Akiongea leo Jumamosi wakati wa hafla ya mazishi katika kijiji cha Iguyio kwenye eneo bunge la Ikolomani katika kaunti ya Kakamega, Mudavadi alisema kuwa upinzani ukiongozwa na kiongozi wao Raila Odinga, unafaa kukubali kwamba kipindi cha uchaguzi kimekamilika na wakati umewadia wa kuwahudumia wakenya.

“Tunaambia upande wa upinzani kwamba, huu si wakati wa maandamano mbali ni wakati wa maendeleo. Tunafahamu changamoto za kiuchumi zinazokumba taifa hili, na hatuna muda wa kupoteza kwa kujihusisha na siasa ambazo hazibadilishi chcochcote wakati huu,”alisema Mudavadi.

Mudavadi alisema kwamba maandamano hayo yanatatiza maendeleo na kuathiri zaidi uchumi wa nchi hii ambao tayari umedorora.

“Wanakimbia kila upande, usiku na mchana, lakini wanafahamu kinaga ubaga kwamba Rais wa Kenya aliyechaguliwa kwa njia halali na kuapishwa ni William Ruto,”alidokeza waziri huyo.

Aliwaonya wale wanaojihusisha katika vitendo vya uhalifu wakati wa maandamano akisema kwamba watachukuliwa hatua za kisheria bila kuzingatia hadhi zao katika jamii.

Wakati huo huo alikariri haja kwa wakenya kuunga mkono sheria ya kifedha akisema itakuwa na manufaa kwa nchi hii.

Alielezea imani kwamba gharama ya juu ya maisha inayoshuhudiwa kwa sasa itashuka hivi karibuni.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *