Mudavadi akabidhiwa Wizara ya Utumishi wa Umma

Martin Mwanje
2 Min Read
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi akikabidhiwa Wizara ya Utumishi wa Umma na Waziri anayeondoka Justin Muturi

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amekabidhiwa mikoba ya kuhumu kama kaimu Waziri wa Utumishi wa Umma. 

Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alikabidhiwa mikoba hiyo na Waziri wa Utumishi anayeondoka Justin Muturi leo Jumanne.

“Namshukuru kila mtu katika Wizara aliyeunga mkono na kuchangia juhudi zetu katika kuimarisha utumishi wa umma. Ilikuwa heshima kuhudumu,” alisema Muturi ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu wa nchi.

Muturi alipigwa kalamu katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais William Ruto kwa serikali yake wiki jana.

Ruto badala yake alimteua mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku kujaza ombwe lililoachwa na Muturi.

Akiwahutubia wanahabari jana Jumatatu katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Ruto alitetea hatua yake ya kumwondoa Muturi kwenye wadhifa huo akisema kuwa Muturi alishindwa kutekeleza majukumu yake.

Ruto alidokeza kuwa alipomteua Muturi kuwa Mwanasheria Mkuu, alitepetea kuwahudumia Wakenya kiasi kwamba ni Muturi mwenyewe aliyemfahamisha Rais kuwa jukumu hilo lilikuwa ngumu kwake.

“Nilipatia JB Muturi kazi kama Mkuu wa Sheria, yeye mwenyewe alinielezea hii kazi kidogo inamlemea, kwa muda nikaona kweli kazi imemlemea, nikampatia kazi ya Waziri,” alisema Rais Ruto.

Ruto alisema, baada ya kutafakari, alimhamisha Muturi na kumteua kama Waziri wa Utumishi wa Umma katika mabadiliko yaliyofanywa mwezi Agosti mwaka 2024.

Hata hivyo, kulingana na Rais Ruto, Muturi alisusia mikutano ya Baraza la Mawaziri, hatua iliyosababisha kutimuliwa kwake.

‘Nilimpatia Bwana Muturi kazi ya kuwa waziri. Hapo katikati akagoma kuja katika Baraza la Mawaziri. Ni mimi nilimfuta kazi au ni yeye alijifuta kazi?,” aliuliza Rais Ruto.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *