Waziri mwenye mamlaka ya juu Musalia Mudavadi, ametoa changamoto kwa klabu ya AFC Leopards kujizatiti na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini msimu huu.
Mudavadi alisema haya Juamato usiku alipokuwa mgeni wa heshima katika hafla za kwanza za mashabiki klabu ya AFC Leopards maarufu kama U45 Unit branch, kuwatuza wachezaji waliotia fora msimu uliopita.
Mudavadi pia alitoa changamoto kwa klabu hiyo kubuni shirika akisisitiza kuwa ndio njia pekee ya kujimudu kifedha bila kutegemea wafadhili.
Mshambulizi Victor Omune alitawazwa mchezaji bora msimu uliopita akiibuka mfungaji bora wa klabu hiyo kwa magaoli 7 na alipokea pia tuzo ya mchezaji bora aliyechaguliwa na wachezaji kila tuzo ikiandamana na zawadi ya shilingi 75,000.
Omune aliisaidia Leopards kumaliza ya tano Ligini na ya tatu katika kombe la shirikisho msimu uliopita katika kombe la Mozzartbet.
Kayci Odhiambo alishinda tuzo ya mchezaji bora aliyechaguliwa na mashabiki iliyoandamana na kitita cha shilingi 85,000.
Mwenyekiti wa Leopards Dan Shikanda, alisema wamejiandaa vyema kwa msimu mpya utakaonza rasmi mwishoni mwa juma hili huku wakilenga kunyakua ubingwa.
Tuzo hizo ziliandaliwa na kundi U45 Unit branch, huku ikitumika kuwajulisha wachezaji waliosajiliwa maajuzi wakiwa :Julius Masaba,Samuel Semo,Sidney Lokale na Peter Maker Manyang Mabok.
Leopards itafungua msimu wa Ligi Kuu msimu wa mwaka 2024/2025, Jumapili hii katika uwanja wa Dandora dhidi ya Mathare united.