Mudavadi ahakikishia wapwani kudumu kwa bandari

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi amehakikishia wakazi wa Pwani kwamba Bandari ya Mombasa itaendelea kuhudumu.

Akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa shule ya upili ya wavulana ya Waa huko Matuga katika kaunti ya Kwale, Mudavadi alipuuzilia mbali matamshi ya wanasiasa fulani wanaodai kwamba serikali inapanga kubinafsisha bandari ya Mombasa.

Mudavadi alisema madai hayo hayana msingi akiongeza kwamba bandari itasalia chini ya usimamizi wa serikali na kuongeza kwamba wanaoeneza uvumi huo wana lengo la kusababisha mkanganyiko na mgawanyiko serikalini.

Kulingana naye, serikali kwa muda sasa serikali imekuwa ikishirikiana na wawekezaji kutoka Japan katika upanuzi wa bandari ya Mombasa ili kuimarisha shughuli zake.

Waziri huyo aliye na mamlaka makuu alisema kwamba serikali haiwezi kuimarisha huduma za bandari pasi na kuwekeza raslimali zaidi na kushirikiana na wawekezaji.

Kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na upinzani, Mudavadi alishangaa ni kwa nini viongozi wa upinzani wamekwenda kortini kupinga ufadhili wa mazungumzo hayo kutoka kwa serikali ilhali wao ndio walitaka mazungumzo yaandaliwe.

Alisema wale ambao wamekimbilia mahakama baada ya kutilia shaka ufadhili wa mazungumzo ya pande mbili wanatumia vibaya haki zao za kikatiba.

Aliwataka wakenya kuwa watulivu na kuipa serikali ya Kenya Kwanza muda wa kufanya kazi akisema ina mpango makhsusi wa kuimarisha uchumi wa taifa.

Sherehe hizo za miaka 100 za shule ya Waa zilihudhuriwa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu, waziri wa uchimbaji madini na uchumi samawati Salim Mvurya, gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani kati ya wengine wengi.

Kwenye hafla hiyo shilingi milioni 28 zilichangwa na zitasaidia kuimarisha muundo msingi shuleni humo.

Share This Article