Serikali inalenga kuongeza muda wa mbio za magari za WRC Safari Rally kutoka siku tatu hadi tano.
Rais William Ruto ameiagiza Wizara ya Michezo kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mbio za Magari, FIA, kufanikisha hatua hiyo.
“Ni wakati wa kutilia maanani ombi la madereva wa Safari Rally la kurejesha siku za mashindano kuwa tano,” alisema Rais Ruto.
Aliyasema hayo siku ya Alhamisi alipoanzisha rasmi mashindano ya mwaka huu ya mashindano ya Safari Rally katika jumba la mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC.
Kiongozi wa taifa alisema kuwa serikali iko makini kutumia vilivyo fursa zinazotolewa na mashindano ya Safari Rally katika ukuaji wa uchumi wa taifa hili.
Kulingana naye, hatua ya taifa hili kuangaziwa na vyombo vya habari vya kimataifa inapiga jeki hadhi ya Kenya.
Anasema hatua hiyo haitawavutia tu watalii, lakini pia wawekezaji ambao watawekeza mabilioni ya fedha katika uchumi wa Kenya na hivyo kupanua fursa kwa wananchi.
“Hii itaimarisha uchumi wa taifa hili, na hivyo kuongeza mapato kwa wanabiashara, kutoa fursa za ajira, kuvutia uwekezaji wa utalii na kupiga jeki huduma za malazi na utoaji huduma zingine.”
Rais aliongeza kuwa mashindano hayo yameratibiwa wakati wa sherehe za Pasaka ili kutoa fursa kwa Wakenya na wageni kushiriki.