Serikali imetangaza kuwa mtihani wa kidato cha nne, KCSE wa katikati ya mwaka utafanywa kuanzia mwaka huu.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba anasema mtihani huo utakuwa ukifanywa mwezi Julai kila mwaka.
“Kuanzia mwaka huu, kufuatia mashauriano ya kina na washikadau, ningependa kutangaza kuwa Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini, KNEC litaanzisha mtihani wa KCSE wa katikati ya mwaka, utakaofanyika mwezi Julai kila mwaka,” alisema Waziri Ogamba wakati akitangaza matokeo ya KCSE ya mwaka jana leo Alhamisi.
“Mtihani huo utawalenga watahiniwa ambao wangependa kufanya tena mtihani wa KCSE, na wale ambao huenda walikosa kuufanya kutokana na ugonjwa au changamoto zingine zisizotarajiwa.”
Waziri aliongeza kuwa watahiniwa ambao ni watu wazima pia wanaweza wakawazia kujisajili kwa ajili ya kufanya mtihani huo wa mwezi Julai.
KNEC imetangaza kuwa itaanza usajili wa watahiniwa wa mtihani wa KPSEA Januari 27, 2025 ilhali usajili wa watahiniwa wa KJSEA na KCSE utaanza Februari 17 mwaka huu.
Mtihani wa mwisho wa KCSE utafanywa mwaka 2027 na wale wenye nia ya kurudia mtihani huo wana hadi wakati huo kufanya hivyo.