Alphonce Felix Simbu ameishindia Tanzania dhahabu ya kwanza mapema leo kwenye mashindano ya riadha Duniani yanayoendelea mjini Tokyo, Japan.
Simbu aliyekuwa amemaliza wa pili katika mbio za New York Marathon mwaka uliopita ameibuka mshindi kwa muda wa saa 2, dakika 9 na sekunde 48, akiandikisha historia kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda dhahabu ya mashindano ya dunia.
Anamal Petros, wa Ujerumani, alishinda medali ya fedha huku shaba ikimwendea Mwitaliano Illias Oouani kwa saa 2, dakika 9, sekunde 53.
Ilikuwa pia mara ya kwanza katika historia ya marathon kwa wanariadha wa kwanza wawili kumaliza kwa muda sawa katika mashindano ya Dunia.