Mtandao wa X utafunga afisi zake nchini Brazil baada ya mvutano wa muda mrefu wa kisheria na jaji mmoja nchini Brazil kuhusu haki na majukumu ya mtandao huo katika kuzuia uenezaji wa habari zisizo sahihi.
Kulingana na tangazo la jana Jumamosi, mtandao huo ambao awali ulifahamika kama Twitter, unafungwa mara moja. Tangazo hilo lilisema pia kwamba watumiaji wa mtanda huo nchini Brazil wanaweza kuufikia.
Kampuni ya X ilisema kwamba jaji wa mahakama ya upeo nchini Brazil Alexandre de Moraes ndiye anawajibikia uamuzi wao.
Hatua hiyo inaashiria mwisho wa mvutano huo wa kisheria kati ya jaji Moraes aliyesema anajaribu kupambana na uenezaji wa habari zisizo sahihi na mmiliki wa X Elon Musk.
Mwanzo wa mwaka huu, Moraes alielekeza mtandao wa X kufunga akaunti fulani zilizolaumiwa kwa kueneza taarifa zisizo sahihi na za chuki, zikiwemo za wafuasi wa aliyekuwa rais wa Brazil Jair Bolsonaro.
Bolsonaro alieneza habari kwamba mfumo wa kielektroniki wa kupiga kura nchini Brazil ulikuwa katika hatari ya kuingiliwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2022.
Miezi kadhaa baada ya uchaguzi huo ambapo alishindwa na Luiz Inacio Lula da Silva, wafuasi wa Bolsonaro walivamia majengo kadhaa ya serikali kulalamikia matokeo.
Jaji Moraes anashikilia kwamba uhuru wa kujieleza haumaanishi uhuru wa uchokozi na kutetea udhalimu.
Kampuni ya X imedai pia kwamba Moraes alimtishia kisiri mmoja wa mawakili wake nchini Brazil kwamba angekamatwa iwapo kampuni hiyo haingefuta maudhui fulani.
Mtandao huo ulichapisha picha za stakabadhi inayoaminika kutiwa saini na jaji Moraes inayosema kwamba wakili Rachel Nova Conceicao angetozwa faini ya kila siku ya dola 3,653 na angekamatwa pia iwapo X haingefuata maagizo ya Moraes.
Mahakama ya upeo nchini Brazil iliambia shirika la habari la Reuters kwamba haitatoa taarifa kuhusu suala hilo na haitathibitisha uhalali wa stakabadhi hiyo.