Bunge kwa ushirikiano na benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF zimezindua mtandao wa bunge kuhusu mashirika hayo mawili wa Kenya.
Hatua hii ni muhimu katika kuimarisha mahusiano kati ya mashirika hayo ya kimataifa na bunge la Kenya.
Inaimarisha pia jukumu la bunge la kukuza uwajibikaji, uwazi na uangalizi bora wa mipango ya maendeleo nchini Kenya inayoungwa mkono na benki ya dunia na shirika la fedha la ulimwengu.
Mtandao huo ulizinduliwa na wanachama wa bodi ya bunge kuhusu mtandao Neema Lugangira mbunge wa Tanzania na Sven Clement mbunge wa Luxembourg.
Humu nchini mtandao huo unaongozwa na mbunge wa Wajir Mashariki Adan Daud, ambaye ni mwenyekiti na seneta mteule Tabitha Mutinda, ambaye ni naibu mwenyekiti.
Qimiao Fan, mkurugenzi wa benki ya dunia katika nchi za Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda, alihudhuria uzinduzi huo ambapo aliangazia ushirikiano wa muda mrefu kati ya Kenya na benki ya dunia.
Mwakilishi wa IMF nchini Kenya, Selim Cakir, naye alikuwepo na alipongeza uzinduzi wa mtandao huo nchini huku akiangazia umuhimu wa wabunge katika kuunda na kufuatilia sera za kiuchumi.
Mtandao huo wa Kenya unatarajiwa kuwa jukwaa la wabunge kuhusiana moja kwa moja na benki ya dunia na shirika la fedha la ulimwengu, kutetea mahitaji ya kipekee ya maendeleo nchini Kenya na kuhakikisha uwajibikaji wa mashirika hayo.