Mswada wa mradi wa nyumba za gharama nafuu utasomwa leo Jumatano kwa mara ya tatu bungeni, baada ya kupitishwa kwenye awamu ya kusomwa kwa mara ya pili jana Jumanne.
Ikiwa utaidhinishwa na theluthi mbili ya wabunge wote watakaokuwa bungeni, basi utakuwa umepitishwa rasmi na bunge la kitaifa na kusubiri kufikishwa katika bunge la seneti.
Kupitishwa kwa mswada huo kutakuwa ufanisi mkubwa kwa serikali ya Kenya Kwanza kwenye azima yake ya kuhakikisha matozo ya ushuru wa nyumba yanaendelea kutekelezwa ili kufadhili mradi huo.
Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula aliwakubali wabunge wanaopendekeza marekebisho kwenye mswada huo kufanya hivyo kabla ya kuanza kwa vikao vya leo alasiri.
Mswada huo mpya uliwasilishwa bungeni baada ya mahakama kuamuru mara mbili kwamba ada ya asilimia 1.5 wanayotozwa wafanyakazi ni kinyume cha katiba.
Majaji walisema ada hiyo haikuwa ya haki kwani ilibagua kwa kutowajumuisha watu wasio katika ajira rasmi na kwamba wananchi hawakuhusishwa kuratibu sheria hiyo.