Mswada wa Mifugo wa mwaka 2024 wakataliwa bungeni

Tom Mathinji
2 Min Read
Mswada wa Mifugo 2024 wakataliwa bungeni.

Bunge la kitaifa limekatalia mbali Mswada wa mifugo wa mwaka 2024, kwa madai kwamba umma haukuhusishwa ipasavyo katika mchakato wa kutayarisha mswada huo.

Uamuzi wa kuutupilia mbali Mswada huo, ulitangazwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wa, aliyesisitiza haja ya kuwahusisha wadau wote katika mchakato wa kuandaa mswada huo.

“Nimemwandikia katibu katika idara ya ustawi wa mifugo, kushirikisha umma katika utayarishaji wa Mswada huo wa mifugo wa mwaka 2024,” alisema Ichung’wa katika kikao cha bunge la taifa Alhamisi alasiri.

Mswada huo wa mifugo 2024, unalenga kustawisha sekta hiyo na kutoa mwongozo kuhusu mazao ya mifugo, utafiti, utoaji mafunzo, kubuni mashirika ya kusimamia mifugo na yale ya kutoa mafunzo.

Mswada huo ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza katika bunge la taifa wakati wowote juma lijalo.

Ichung’wa alikiri kuwa Mswada huo wa mifugo 2024, umeibua wasiwasi miongoni mwa Wakenya, akisema kuwa;”Tumesikiliza wasiwasi wa Wakenya kuhusu Mswada wa mifugo 2024 na umma unafahamu madhara yanayotokana na Mswada huo una fursa ya kuchangia katika mswada huo,”.

Katibu katika idara ya ustawi wa mifugo, amejukumiwa kushirikisha wadau mbali mbali wakiwemo wafugaji, viwanda vinavyohusika na mifugo pamoja na makundi ya kijamii ili kupokea maoni yao kuhusu Mswada huo.

Wizara ya Kilimo inatarajiwa kuwasilisha ripoti kwa bunge la taifa, kuelezea matokeo ya ushirikishi wa umma.

Ichung’wa alisema hatma ya mswada huo wa Mifugo, utategemea matokeo kuhusu ushirikishi wa umma.

Share This Article