Kamati ya Seneti inayohusika na maswala kisheria na haki za binadamu, imekataa mswada unaotaka kuongeza muda wa kuhudumu kwa kwa viongozi waliochaguliwa humu nchini.
Mswada huo ulipendekeza kuongezwa kwa muda wa kuhudumu kwa viongozi waliochaguliwa ikiwa ni pamoja na muda wa kuhudumu kwa Rais, kutoka miaka tano hadi saba.
Hii imefuatia pingamizi kali dhidi ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Hillary Kiprotich Sigei alisema asilimia 99.99 ya wakenya waliowasilisha maoni yao walipinga vikali mapendekezo hayo ya kurekebisha Katiba.
Sigei alisema kuwa Kamati hiyo ilizingatia kwa makini maoni yote ya umma kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria.
Seneta wa Nandi Samson Cherargey aliwasilisha mswada huo unaotaka kuongeza muda wa kuhudumu kwa viongozi waliochaguliwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba ukiwemo muda wa kuhudumu wa magavana na wabunge.
Mswada huo pia ulikuwa ukipendekeza kuundwa kwa ofisi ya Waziri Mkuu ambaye atateuliwa na rais.