Mswada wa Fedha ndio msingi wa serikali, asema Mudavadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema ikiwa serikali ingeshindwa kupitisha Mswada wa Fedha 2024, hatua hiyo ingetumiwa kuharamisha serikali ya Rais William Ruto.

Waziri huyo wa mambo ya nje alisema mjadala unaoendela sasa kuhusu mswada huo licha ya kuwa ni wa kiuchumi, pia ni wa kisiasa.

“Mswada wa Fedha ndio msingi wa serikali. kimataifa, iwapo mswada wa fedha utashindwa, madhara yake ni kwamba serikali imeng’olewa madarakani. Ni sawa na kura ya kutokuwa na imani na serikali. Si mchezo,” alisema Mudavadi.

Kulingana na Mudavadi, wanachama wa upinzani wanafahamu vyema swala hilo, na walikuwa makini kutekeleza hilo iwapo mswada huo ungeshindwa katika bunge la taifa.

“Hawa watu (wa Upinzani) wanaisukuma wanasema tu ni mambo ya fedha. Mkiangusha mswada wa fedha kwa serikali yeyote, litakalofuatia ni kutokuwa na imani na serikali, hivyo kutimuliwa kwa serikali iliyoko na uchaguzi mkuu kuandaliwa,” alidokeza Mudavadi.

Mudavadi aliyewaongoza viongozi wa chama cha UDA katika kukagua miradi ya maendeleo eneo la Eldama Ravine kaunti ya Baringo, alisema swala ya Mswada wa Fedha halipaswi kuchukuliwa kwa urahisi.

“Watu wanapanga kuangusha Mswada wa Fedha 2024, ili waseme hawana imani na Rais William Ruto ndio aende nyumbani. Msichukulie swala hili kwa urahisi, msichukulie kama mzaha,” alisema Mudavadi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *