Wabunge siku ya Alhamisi walipiga kura na kupitisha mswada wa fedha wa mwaka 2024, baada ya kusomwa kwa mara ya pili.
Wabunge 204 walipiga kura kuunga mkono mswada huo, dhidi ya wabunge 115 walioupinga baada ya mjadala mkali bungeni.
Mswada huo sasa utajadiliwa na kamati ya bunge lote, ambapo wabunge wataangazia mapendekezo yaliyotolewa.
Kamati ya bunge lote litajadili kifungu baada ya kingine, kisha kila kifungu kitapigiwa kura kabla ya ripoti kuwasilishwa bungeni kuidhinishwa.
Iwapo ripoti hiyo itaidhinishwa, mswada huo utasomwa mara ya tatu bungeni. Katika awamu ya tatu hakuna marekebisho ambayo yatafanyiwa mswada huo.
Mswada huo ukipigiwa kura baada ya kusomwa mara ya tatu, spika wa bunge la taifa atawasilisha mswada huo kwa Rais kutiwa saini kuwa sheria.
Rais huwa na muda wa siku 14 kutia saini mswada huo kuwa sheria au kuirejesha bungeni kwa marekebisho zaidi.