Usafiri jijini Nairobi unatazamiwa kutatizika kwa kiwango kikubwa kuanzia leo Jumatatu wakati Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi liking’oa nanga.
Msongamano mkubwa wa magari unatarajiwa kushuhudiwa wakati barabara muhimu jijini humo zitakapofungwa kuanzia leo Jumatatu hadi keshokutwa Jumatano.
Barabara zitakazofungwa ni pamoja na ni ile ya Harambee Avenue kutoka mzunguko wa Parliament hadi makutano ya barabara ya Taifa, barabara ya Taifa kutoka makutano ya Harambee Avenue hadi makutano ya City Hall Way, makutano ya barabara ya City Hallway kutoka mzunguko wa Holy Family Basilica hadi makutano ya barabara ya Taifa na barabara ya Parliament kutoka mzunguko wa Harambee Avenue hadi mzunguko wa City Hallway.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha usafiri usiokuwa na doa wa wajumbe wapatao 30,000 wanaotarajiwa kuhudhuria kongamano hilo la siku tatu litakalomalizika keshokutwa Jumatano.
Msongamano wa magari unatarajiwa kushuhudiwa kwwenye barabara kuu za kuingia na kutoka jijini Nairobi kwa sababu wengi wa wageni watakaohudhuria kongamano hilo wataishi kwenye hoteli zilizo kwenye barabara hizo.
Wengi wamekodisha mahali pa kulala kwenye barabara ya kuelekea Thika, ile ya Ngong, ya kuelekea Mombasa na ya kuelekea Limuru kati ya nyingine.
Megesho ya magari jijini Nairobi kama vile ya KenyaRe, Mahakama ya Upeo, Holy Family Basilica na Charter Hall yamefungwa kwa matumizi ya umma na yatatumiwa na wageni wa kongamano.
Rais Wiliam Ruto leo Jumatatu anatarajiwa kufungua rasmi Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi litakalofanyika katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC.