Huku sehemu nyingi za nchi zikishuhudia kiwango kikubwa cha mvua, wananchi wametakiwa kuwa makini, kwa kuwa mvua hiyo inaweza kusababisha mafuriko.
Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki amesema mabwawa ya kuzalisha nguvu za umeme ya Seven forks yamejaa pomoni, na maji yake yameanza kutiririka.
Kupitia kwa taarifa leo Jumatano, waziri Kindiki alisema maeneo yaliyo karibu na maziwa mito, nyanda za chini, na maeneo yaliyo na mifumo duni ya maji taka, huenda yakafurika na wanaoishi maeneo hayo wanashauriwa kuhamia maeneo salama.
Waziri alisema jamii zinazoishi karibu na maziwa na mito katika maeneo ya HomaBay, Siaya, Busia, Nyando, Nyakach na Muhoroni huenda zikakumbwa na mafuriko.
Hata hivyo, Prof. Kindiki alisema serikali imeweka mikakati ya kukahikisha usalama wa umma. Alisema maeneo ya nyanda za chini huko maeneo Migori, Kakamega, na Vihiga huenda yakafurika ikiwa kiwango cha mvua katika sehemu hizo kitaongezeka.
Kulingana na waziri huyo, shirika la msalaba mwekundu humu nchini na mashirika husika ya kitaifa na ya kimataifa yameahidi kushirikiana na serikali kukabiliana na athari za mafuriko.